Mafuriko ya karibuni nchini Somalia yameua watu 29 na kupelekea wengine laki tatu kupoteza makazi
Afisa mmoja wa nchi hiyo amesema, mafuriko hayo makubwa yaliyotokea kusini-magharibi mwa Somalia yamepelekea mamia ya maelfu ya watu kuhama makazi yao, huku mvua kubwa za El Nino zikiendelea kunyesha Afrika Mashariki.
Tangu mwanzoni mwa mwezi huu, mvua kali zimeikumba Somalia na majirani zake Kenya na Ethiopia, na kusababisha maporomoko ya ardhi na kuzamisha vijiji na mashamba.
Mafuriko hayo yanakuja baada ya Somalia na baadhi ya maeneo ya Ethiopia na Kenya kukumbwa na ukame mkubwa kuwahi kushuhudiwa katika eneo hilo katika miongo minne iliyopita.
Tulionya mapema kuhusu mvua hizi na tukatabiri hali hii , Mohamed Moalim Abdullahi, mwenyekiti wa Shirika la Kukabiliana na Majanga la Somalia, alisema Jumanne jioni.