Umoja wa Afrika (AU) umetoa wito kwa wadau wa umma na binafsi barani Afrika kufanya juhudi za pamoja ili kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya.
Taarifa iliyotolewa na Umoja huo inasema wito huo umetolewa na kaimu ofisa mwandamizi wa Umoja wa Afrika Bibi Angela Martins, wakati akihutubia mashauriano ya wataalam wa kiufundi wa bara kuhusu kupunguza mahitaji ya dawa.
Bibi Martins amesema licha kuwa ya juhudi za kupambana na ulanguzi na usambazaji wa dawa za kulevya ni muhimu, pande nyingine za tatizo hilo pia zinatakiwa kuzingatiwa kama vile kuzuia watu kutumia, matibabu, urekebishaji, na kujumuishwa tena kwenye jamii, mchanganyiko huu unaweza kuvunja mzunguko mbaya wa matumizi ya dawa za kulevya na utegemezi wake.
Amesisitiza umuhimu wa mazungumzo, kubadilishana ujuzi, na ushirikiano kati ya wataalam, watunga sera, mashirika ya kiraia, na wadau, akitambua kwamba hakuna nchi inayoweza kukabiliana na tishio la dawa za kulevya peke yake.