Raia wa Kenya wameonekana kukerwa na hatua ya mamlaka kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki kutangaza ada kwa vitambulisho vya kitaifa.
Wakaazi nchini humo wamekuwa wakipata vitambulisho bila malipo wanapohitimu umri wa miaka 18 ila kwa sasa watahitajika kulipa ada ya shillingi elfu moja pesa ya taifa hilo ambazo ni sawa na $6 au £5.
Aidha raia ambao wamepoteza vitambulisho vyao vya kitaifa sasa watahitajika kulipa shillingi elfu mbili pesa ya Kenya.
Mabadiliko hayo mapya ambayo yanakuja wakati huu ambapo raia wa Kenya wanakabiliwa na ugumu wa maisha, yamekashifiwa vikali kwenye mitandao ya kijamii nchini humo.
Kando na vitambulisho vya kitaifa, mabadiliko hayo mapya pia yameonekana kuathiri sekta nyengine ikiwemo passpoti za usafiri, vyeti vya ndoa, stakabadhi za kazi, vyeti vya kuzaliwa pamoja na vile vya mazishi.