Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema magari ya Kliniki Tembezi (Mobile Clinic) yakatumike katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) hususani kuibua wagonjwa wapya, UKIMWI pamoja na Malaria.
Waziri Ummy amesema hayo leo Novemba 8, 2023 wakati wa makabidhiano ya magari hayo ya Kliniki Tembezi yenye thamani ya Mil. 618,477,000/= yaliyofanyika Mkoani Dodoma.
“Karibu 35% ya wagonjwa wa Kifua Kikuu bado tunao katika majumba yetu, ofisi zetu, vijiji vyetu na mitaani kwetu, Kwahiyo naamini kabisa magari haya yatatumika katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa TB kwa kuibua wagonjwa wapya, mapambano dhidi ya Malaria na UKIMWI”. Amesema Waziri Ummy
Aidha, Waziri Ummy amesema magari hayo (Mobile Clinic) yatakuwa yanatoa huduma za Afya za kisasa katika jamii ambayo ipo mbali na huduma za Afya pamoja na kutembea katika masoko na stendi za magari kutoa huduma za upimaji.
“Magari haya pia yatumike kutoa huduma za chanjo kwa watoto ambao wanapaswa kupata chanjo, pia yakatumike kwenye mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza na mtu akikutwa na changamoto basi aambiwe aende kwenye kituo cha kutoa huduma za Afya kwa matibabu zaidi”. Amesema Waziri Ummy
Aidha Waziri Ummy amesema, Tanzania ina changamoto ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo Kisukari ambapo katika kila watu 100 wenye umri wa miaka 15 na kuendelea watu 9 wana ugonjwa wa Kisukari, changamoto ya watu wenye Shinikizo la Juu la Damu ambao ni 25% na hawajui.
“Nitoa shukrani nyingi sana kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujali Afya za Watanzania kwa kuendeleza mashirikiano na Mataifa mbalimbali na kuja kuwekeza nchini hasa katika Sekta ya Afya”. Amesema Waziri Ummy