Tottenham Hotspur wamethibitisha kuwa James Maddison amelazimika kujiondoa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Uingereza kwa ajili ya mechi za kimataifa za mwezi Novemba.
Maddison alipata jeraha la kifundo cha mguu bila kugusa wakati Spurs walipochapwa 4-1 na wapinzani wao Chelsea Jumatatu usiku.
Ingawa Spurs hawajafichua ukubwa wa tatizo la Maddison kwa sasa, wametangaza kuwa hatajiunga na Three Lions kwa ajili ya mechi za kimataifa mwezi huu.
“Tunaweza kuthibitisha kwamba James Maddison ameondolewa kwenye kikosi cha Uingereza kutokana na jeraha la kifundo cha mguu,” Tottenham ilisema katika taarifa.
“Kiungo huyo hatashiriki katika mechi za kufuzu kwa UEFA EURO 2024 za Three Lions dhidi ya Malta na Macedonia Kaskazini, na atasalia Hotspur Way kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati na madaktari wa Klabu.”
Kocha mkuu wa Tottenham Ange Postecoglou huenda akatoa taarifa kuhusu utimamu wa Maddison kwenye mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa kabla ya safari ya wikendi hii kuelekea Wolves.