Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (WHMTH) imeingia hati ya mashirikiano (MoU) na Serikali ya Jamhuri ya Korea kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani na Usalama (WMDU) kuhusu ushirikiano katika utekelezaji na matumizi ya Mfumo wa Anwani za Makazi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Utiaji saini wa hati hiyo umefanyika nchini Korea Kusini.
Hati hiyo imesainiwa na Bw. Mohammed Khamis Abdulla, Katibu Mkuu wa WHMTH kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Dkt. KO Kidong, Makamu wa Waziri wa WMDU kwa niaba ya Jamhuri ya Korea.
Lengo la hati ya mashirikiano ni kushirikiana katika utekelezaji na matumizi ya Mfumo wa Anwani za Makazi kwa kipindi cha miaka mitano. Katika kipindi hicho, shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na kubadilishana ujuzi na uzoefu, utekelezaji na matumizi ya Mfumo, kuboresha Mfumo wa Kidijitali unaojulikana kwa jina la NaPA, kujenga uwezo kwa wataalam wa ndani, na kushirikiana katika kuhamasisha na kutoa elimu kwa umma.
Hii ni hatua muhimu katika kuimarisha mfumo wa anwani za makazi nchini Tanzania na kuleta maendeleo katika sekta ya habari, mawasiliano, na teknolojia ya habari. Ushirikiano huu utasaidia katika urahisi wa mawasiliano na upatikanaji wa huduma kwa wananchi.