Mradi wa kuendeleza utalii kusini (REGROW) utaendelea kuimarisha uhifadhi wa misitu na kuinua uchumi kwa wananchi wa nyanda za juu kusini kupitia ufugaji nyuki.
Haya yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula (MB) wakati akijibu swali la Mbunge wa Iringa Mjini Mhe. Jesca Jonathani Msambatavangu ambaye alitaka kujua je Serikali haioni umuhimu wa kugawa mizinga ya nyuki ili kubadili shughuli za kiuchumi zinazoharibu mazingira kama kukata miti na mkaa Iringa?
Mhe Kitandula alifafanua kuwa Serikali kupitia Mradi wa REGROW imetoa elimu ya Ufugaji nyuki kwa jamii ya Tungamalenga na kwa mwaka wa fedha 2023/2024 imepanga kugawa mizinga 50 kwa kikundi cha SUBIRA kilichopo Wilaya ya Iringa.
Vilevile Mhe. Kitandula amesema kuwa Elimu ya ufugaji Nyuki imeendelea kutolewa kwa jamii zinazozunguka hifadhi ambapo kupitia elimu hiyo wananchi wamefundishwa namna bora ya kufanya shughuli za ufugaji nyuki kwa tija.
“Mwaka wa fedha 2022/2023 Wizara ilitoa mizinga 269 yenye thamani ya shilingi milioni 26.9 kwa vikundi 19 vya wafugaji nyuki katika Wilaya za Iringa, Kilolo na Mufindi” Aliongeza Mhe. Kitandula
Aidha Mhe. Kitandula amesema kwamba Mfuko wa Misitu Tanzania umetoa ruzuku ya Shilingi Million 20 kwa vikundi 2 vya ufugaji Nyuki vilivyopo Wilaya ya Iringa lakini pia umekuwa ukitoa tangazo na kupokea maombi ya ruzuku zitolewazo kwa wadau wa misitu na ufugaji nyuki na sasa unaendelea kupokea maombi ya ruzuku.