Taasisi ya SELF HELP AFRICA katika hafla yake iliyofanyika Jijini New York Nchini Marekani ikuhusu biashara Afrika, imemtunukia Tuzo Mwanamitindo Mtanzania Flaviana Matata kutokana na juhudi zake kubwa za kuwasaidia Watoto wa kike kupata elimu pamoja na kuwawezesha kwa ujumla Wanawake na Watoto wa kike nchini Tanzania kupitia Taasisi ya @FlavianaMatataFoundation.
Flaviana ambaye pia alipata nafasi ya kuzungumza mbele ya hadhira iliyokusanyika katika tukio hilo ameshukuru kutunukiwa Tuzo hiyo ya 2023 Empowering Africa Award na kueleza yafuatayo.
“Wikendi iliyopita nilitunukiwa na @selfhelpafrica kwa kazi tunayofanya Tanzania, kupokea Tuzo ya 2023 Empowering Africa Award kutoka kwa Taasisi kama hii ni heshima kubwa, Tuzo hii si yangu tu na Timu bali ninaipokea kwa niaba ya wengine wanaobadilisha maisha barani Afrika.
“Chumba kilijaa Watu waliokusanyika kusherehekea kwa madhumuni ya pamoja, kuwekeza katika mustakabali wa Wajasiriamali wa Kiafrika wa Vijijini haswa Wanawake wastahimilivu ambao wanaunda uti wa mgongo wa Jumuiya hizi, juhudi zao sio biashara tu… ni njia za maisha kusaidia familia, kufadhili huduma za afya, elimu na makazi kupitia usaidizi wa pamoja tutaendelea kupanda mbegu za mabadiliko na kuhakikisha mzunguko wa maendeleo unaendelea kustawi” ——— ameandika @FlavianaMatata.