Hamas imetangaza siku ya Jumapili kuwa inasitisha mazungumzo kuhusu mateka kutokana na hali ilivyo katika hospitali ya Al-Shifa huko Gaza, afisa wa Palestina aliye karibu na mazungumzo kuhusu mateka ameliambia shirika la habari la REUTERS.
Hospitali hiyo ililengwa na mashambulizi makali hivi karibuni, wakati wanajeshi wa Israel wakikaribia hospitali hiyo.
Israel inaishutumu Hamas kwa kutumia hospitali hiyo kama kamandi yake bila kutoa uthibitisho. Hamas imekanusha shutuma hizi.
Hayo yanajiri wakati mapigano yanaendelea kwenye mpaka na Israel na kusini mwa Lebanon, ambako kundi la waislamu Washia wenye silaha Hezbollah lina makao yake makuu.
Jeshi la Ulinzi la Israel limesema makombora ya vifaru yalirushwa na Hezbollah siku ya Jumapili na kugonga maeneo kadhaa yanayokaliwa na raia ndani ya Israel.
IDF ilisema ilikuwa inalipiza kisasi kutokana na mashambulizi ya risasi kutoka Lebanon.