Watu wasiopungua sita wameuawa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika mzozo baina ya jeshi na wanamgambo wanaofungamana na serikali.
Tukio hilo lilijiri Jumamosi jioni katika Kijiji cha Mugerwa yapata kilomita 15 kutoka mji wa Goma. Afisa mmoja wa usalama ambaye hakuta jina lake litajwe amesema wanajeshi walifyatuliana risasi na wanamgambo wanaojulikana kama Wazalendo na kwamba mapigano hayo yalisababisha vifo vya watu sita.
Hayo yamejiri baada ya mapigano mapya ya hivi majuzi kati ya askari wa serikali ya Kongo na waasi wa M23 ambayo yanaonyesha kuendelea kwa tishio linalosababishwa na ukosefu wa usalama mashariki mwa nchi.
Mapigano hayo yanajiri wakati kuna msukumo mkuu wa shughuli za kisiasa nchini DRC ukilenga uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Disemba.
Tangu mwaka wa 2021, M23, moja ya makundi kadhaa yenye silaha yanayopigana mashariki mwa Kongo, limeteka maeneo mengi katika jimbo la Kivu Kaskazini.
Katika matukio ya hivi punde zaidi, mapigano yameripotiwa ndani na karibu na eneo linalodhibitiwa na M23 la Wilaya ya Masisi ya Mkoa wa Kivu Kaskazini karibu na mpaka wa Rwanda na Uganda, baada ya miezi sita ya utulivu hafifu.