Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewataka vijana wenye rika balehe (hasa wasichana) kuepuka vishawishi kama chipsi na vingine ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya VVU na UKIMWI.
Waziri Ummy ambae pia ni mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini amesema hayo wakati akifunga kampeni ya Jikubali katika viwanja vya Usagala, Halmashauri ya Jiji la Tanga ikiwa ni tayari imeshazifikia Halmashauri 18 za MIkoa mbalimbali ikiwemo Dodoma.
“Wanangu, njia za kupata maambuzi ya VVU na UKIMWI zipo nyingi lakini epukeni vishawishi kama chipsi kwa kuwa chipsi ni chakula Kama vyakula vingine, tusikubali kudaganyika kwa vishawishi vyovyote vile.” Amesema Waziri Ummy
Aidha, Waziri Ummy amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imepanga kutokomeza VVU na UKIMWI ifikapo mwaka 2030 ambapo imelenga kuwa na Sifuri Tatu katika maeneo ya maambukizi mapya, vifo na unyanyapaa.
“Kampeni hii ya JIKUBALI itatusaidia kwa kiwango kikubwa kama nchi kufikia malengo makuu ya kutokomeza VVU na UKIMWI ifikapo mwaka 2030 ambapo tumelenga kuwa na sifuri tatu katika maeneo ya maambukizi mapya, vifo na unyanyapaa.” Amesema Waziri Ummy
Waziri Ummy ameongeza kuwa takwimu za utafiti wa viashiria vya UKIMWI nchini iliyofanyika mwaka 2016-2017 zinaonyesha hali ya maambukizi iko juu zaidi kwa vijana wa kike, ukilinganisha na wa kiume.
Amesema, kwa vijana wenye umri kati ya miaka 10 hadi 14, asilimia 0.3 wa kike na asilimia 0.3 wa kiume wanaishi na maambukizi ya VVU, wenye umri kati ya miaka 15 hadi 19 wa kike ni asilimia 1.0 na wakiume ni asilimia 0.4 na kwa wale wenye umri kati ya miaka 20 hadi 24 wa kike ni asilimia 3.4 wa kiume ni asilimia 0.9.