Takriban wagonjwa 32 wa hospitali ya al Shifa ya Gaza wamefariki katika muda wa siku tatu zilizopita, msemaji wa wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas amesema.
Waliofariki ni pamoja na watoto watatu waliozaliwa kabla ya wakati, Ashraf al Qidra alisema.
Operesheni katika hospitali hiyo kubwa zaidi katika eneo la Palestina, ilisitishwa siku ya Jumamosi baada ya kukosa mafuta ya jenereta zake, kumaanisha vifaa vya kuokoa maisha kama vile incubators haziwezi kufanya kazi.
Israel ilisema ilikuwa imeacha lita 300 za mafuta karibu na hospitali hiyo lakini Hamas walikataa – ingawa awali Bw al Qidra alikanusha matoleo ya mafuta yalikataliwa na kusema lita 300 zingefanya hospitali iendelee kwa nusu saa tu.
Aliiambia Reuters lita 8,000 hadi 10,000 zinahitajika kwa siku na akasema zinapaswa kuwasilishwa na Shirika la Msalaba Mwekundu au shirika lingine la misaada.
Hospitali nyingine katika Mji wa Gaza, al Quds, ililazimika kufungwa hapo jana kwa sababu iliishiwa na mafuta.
Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina, linaloendesha kituo hicho, limesema kuwa vikosi vya Israel viko karibu na matayarisho ya kuwahamisha wagonjwa 6,000, matabibu na watu waliokimbia makazi yao.