Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi katika vijiji vya Mwadila, Zabazaba na Igongwa katika halmashauri ya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu.
Akieleza mbele ya wakazi wa vijiji hivyo Mwenyekiti wa Kamati ya ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mzava wakati wa Ziara ya kamati hiyo wilayani humo amesema ni jambo la kuipongeza Wizara ya Ardhi katika kuwezesha mradi huo kuweka mazigira mazuri ya matumizi bora ya ardhi.
Amesema kuwa kazi ya kamati hiyo ambayo wamekuja kuifanya ni kufuatilia na kujiridhisha fedha zilizotolewa na Rais Dkt Samia Suluhu baada ya kupitishwa na bunge ili kutekeleza mradi huo zilizotengwa kwa wilaya ya Maswa zimefika na zimefanya kazi iliyokusudiwa.
Amesema kuwa kulingana na maelezo waliyoyapata kutoka kwa watekelezaji wa mradi huo pamoja na wananchi wa vijiji hivyo sambamba na kuonyesha ramani zilizotengwa kwa ajili ya kuonyesha matumizi bora ya ardhi kwa pamoja wamejiridhisha kuwa kazi imefanyika vizuri.
“Kazi yetu sisi kamati hii ya bunge ambayo imetufikisha wilayani Maswa ni kufuatilia na kujiridhisha fedha zilizotolewa na bunge zaidi ya Tsh. Bilioni 3 kwa ajili ya kutekeleza mradi huu katika wilaya hii zimefika na kufanya kazi iliyokusudiwa kwa ufanisi.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi mhe. Geophrey Pinda amesema kuwa wilaya hiyo inakwenda kupima vijiji vyote 120 kwa mchanganuo kuwa vijiji 106 vitapimwa, Vijiji 5 vitaingizwa katika mji wa Maswa na vijiji 9 vitapewa hadhi ya kuwa miji midogo na wananchi watapatiwa Hati Milki za Ardhi.
Amesema kuwa mradi huo utakuwa endelevu na moja ya umuhimu wa kupima miji ni kuweka matumizi bora ya ardhi na kuondoa changamoto zilizokuwa zinajitokeza za migogoro ya ardhi ya mara kwa mara.
Amesema Wizara yake imeweza kutenga Hekta 77,000 kwa ajili ya kilimo cha Umwagiliaji, Hekta 481 kwa ajili ya taasisi za serikali na Hekta 713 kwa ajili ya kuweka Viwanda na Uwekezaji.