Rais wa DRC, Félix Tshisekedi ametoa hotuba yake kuhusu hali ya taifa lake hapo jana Jumanne, kuashiria hitimisho la muhula wa kwanza wa miaka mitano wa urais wake. Hotuba hii iliaagazia pakubwa mafanikio ya serikali yake katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Kwa zaidi ya saa mbili, rais Tshisekedi alifanya tathmini ya mambo yaliotekelezwa chini ya uongozi wake na yale ambayo bado yanasalia kutekelezwa.
Mkuu huyo wa nchi pia aliwakumbuka na kuwaenzi wahanga wa ghasia zinazoendelea mashariki ya taifa lake, pia akieleza masikitiko yake kuhusu ongezeko la vurugu katika baadhi ya mikoa.
Kuhusu usalama, alikaribisha uamuzi wake wa kuanzisha hali ya dharura katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri. Ingawa hatua hii ya kipekee bado haijarejesha usalama kikamilifu, imesaidia kupunguza wizi wa madini na forodha na vyanzo vya migogoro, alisisitiza rais.
Rais pia alizungumzia hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa barabara na ukarabati wa miundombinu ya barabara na kutoa ahadi mpya katika sekta hiyo.