Kinara wa upinzani nchini Liberia, Joseph Boakai yupo mbele kwenye matoke ya awali ya duru ya pili ya uchaguzi rais kati yake na Rais George Weah anayegombea muhula wa pili.
Kwa mujibu wa matokeo ya awali ya Kamisheni ya Uchaguzi ya Liberia, Boakai kufikia sasa anaongoza kwa asilimia 50.71, huku Weah akipata asilimia 49.29 ya asilimia 22.3 ya kura zilizohesabiwa kufikia sasa.
Wananchi wa Liberia walipiga kura juzi Jumanne katika duru ya pili ya uchaguzi huo unaowachuanisha Rais George Weah na Makamu wa Rais wa zamani Joseph Boakai baada ya mchuano mkali wa duru ya kwanza, ambapo hakuna aliyeweza kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura.
George Weah, 57, aliongoza kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi huo mwezi Oktoba, kwa kupata asilimia 43.83 ya kura, na Boakai alipata asilimia 43.44.
Boakai, 78, ni mwanasiasa mkongwe ambaye kuanzia mwaka 2006 hadi 2018 alikuwa naibu wa Ellen Johnson Sirleaf, rais wa kwanza mwanamke barani Afrika kwa kuchachaguliwa kidemokrasia.
Katika uchaguzi wa mwaka 2017 George Weah ambaye ni mchezaji soka mashuhuri wa zamani alishinda kwa zaidi ya asilimia 61 ya kura.
Huu ni uchaguzi wa nne wa rais baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo lakini wa kwanza bila ya kuwepo ujumbe wa Umoja wa Mataifa.