Shirika la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu la Umoja wa Mataifa (OCHA) Jumatano lilisema licha ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan na mapambano ya kutoa huduma za afya, hali ya mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu imekuwa mbaya zaidi nchini humo.
OCHA ilisema ripoti kutoka Wizara ya Afya ya Sudan na Shirika la Afya Duniani (WHO) ilionyesha kuwa, hadi tarehe 12 Novemba watu takriban elfu tatu wanaoshukiwa kuambukizwa ugonjwa wa kipindupindu wameripotiwa kwenye majimbo saba kati ya majimbo yote 18, na watu 89 kati yao wamefariki, idadi ambayo ni maradufu ya ile iliyoripotiwa chini ya wiki tatu zilizopita.
OCHA ilisema Umoja wa Mataifa na washirika wa kibinadamu wanaongeza nguvu ya kukabiliana na janga hilo, ikiwa ni pamoja na kuunga mkono upimaji na matibabu kwa watu walioambukizwa, na kwamba kampeni za kupata chanjo zinatarajiwa kuanza kufanyika mwishoni mwa Novemba kwenye majimbo yaliyoathiriwa.