Watumishi wa maabara ya Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila wametakiwa kutumia mikutano yao ya kila mwaka kujadili na kupanga mikakati itakayosaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuboresha hali ya utoaji huduma.
Kauli hiyo imetolewa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji na Naibu Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila Dkt.Julieth Magandi wakati akifungua mkutano wa wadau wa maabara uliofanyika leo MNH-Mloganzila.
“Wizara ya Afya iliweka mikakati mbalimbali ya kuboresha huduma za maabara nchini kufikia kiwango cha kimataifa yaani ithibati ya ubora kimataifa. Maboresho hayo yalilenga kuboresha nav kuimarisha huduma za kimatibabu ya afya nchini Tanzania” ameongeza Dkt. Magandi
Dkt. Magandi amewasisitiza wataalam hao kuzingatia na kuzijadili mada zinazowasilishwa kikamilifu na baada ya hapo kuwashirikisha wataalam wengine maazimio yalifikiwa na hatimaye wote kwa pamoja kuyatekeleza.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Shirikishi MNH-Upanga & Mloganzila Dkt. Mbonea Yonazi amesema kikao hicho kinalenga kupitia utendaji kazi wa maabara na kuweka mikakati anuai kwa kuzingatia kuwa maabara ni kitovu cha utoaji huduma za tiba hospitalini.
Dkt. Mbonea amebainisha kuwa kikao hicho kimeshirikisha wadau mbalimbali wanaochangia katika kufanikisha utoaji wa huduma za maabara kwa ufasaha ikiwemo idara mbalimbali za tiba (clinical services), Idara ya Fedha na Mipango, Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Kitengo cha Ugavi na Kitengo cha Mawasiliano.
Katika kikao hicho mambo mbalimbali yatajadiliwa ikiwemo kupata taarifa za utekelezaji wa majukumu katika kipindi 2022/23, kupata takwimu halisi ya maoni ya wateja na malalamiko yao, kuangalia maeneo yenye upungufu na namna ya uboreshaji, kuangalia tathmini ya wazabuni wanaotoa huduma ndani ya Maabara kwa kipindi cha mwaka 2022/23 pamoja na kutathmini gharama za uendeshaji pamoja na mapato ndani ya idara