Afrika Kusini imewasilisha rufaa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa ajili ya uchunguzi kuhusu madai ya uhalifu wa kivita uliofanywa na Israel huko Gaza, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alisema.
Hatua hiyo inajiri huku wabunge wa Afrika Kusini wakitarajiwa kujadili hoja siku ya Alhamisi ya kutaka Ubalozi wa Israel nchini Afrika Kusini ufungwe na kukatwa uhusiano wote wa kidiplomasia na nchi hiyo hadi ikubali kusitishwa kwa mapigano.
Ramaphosa alisema nchi yake inaamini kuwa Israel inafanya uhalifu wa kivita na mauaji ya halaiki huko Gaza, ambako maelfu ya Wapalestina wameuawa na hospitali na miundombinu ya umma imeharibiwa.
“Kama Afrika Kusini, kwa hiyo, pamoja na nchi nyingine nyingi duniani, tumepeleka hatua hii yote ya serikali ya Israel kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu,” Ramaphosa alisema Jumatano wakati wa ziara ya kitaifa nchini Qatar.
“Tumetuma rufaa kwa sababu tunaamini kuwa uhalifu wa kivita unafanywa huko. Na bila shaka hatuungi mkono hatua zilizochukuliwa na Hamas hapo awali, lakini vile vile tunalaani vitendo vinavyoendelea hivi sasa na tunaamini kwamba vinahitaji uchunguzi wa ICC,” aliongeza.