Rais wa Malawi Lazarus Chakwera ameamua kupiga marufuku kwa muda safari za nje kwa serikali yake na yeye mwenyewe, ili kuisaidia nchi yake kupunguza matumizi katika kukabiliana na mzozo wa kiuchumi. Hatua hiyo imetangazwa baada ya IMF kuidhinisha mkopo wa dola milioni 175.
“Ninatangazwa kusitishwa kwa safari zote za nje zinazofadhiliwa na Serikali kwa maafisa wake wote katika ngazi zote (…) hadi mwisho wa mwaka wa fedha mwezi Machi,” ametangaza Lazarus Chakwera kwenye televisheni.
Chakwera, mhubiri wa zamani wa kiinjilisti, kwa hivyo hataenda kwenye mkutano wa kilele wa tabianchi, COP28, uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi wa Novemba katika Umoja wa Falme za Kiarabu.
Pia aliagiza wajumbe wote wa serikali yake walioko katika safari za kikazi nje ya nchi kuharakisha kurejea nyumbani, na kupunguzwa kwa nusu ya bajeti ya mafuta ya maafisa wakuu wa serikali.
Malawi, nchi isiyo na bandari kati ya Msumbiji, Tanzania na Zambia, ilitangaza wiki hii kushuka kwa thamani ya asilimia 44 ya sarafu yake ya Kwacha, ili kuweza kupata mkopo wa IMF.
Nchi imetatizika kwa miongo kadhaa kufikia ukuaji endelevu licha ya kupokea bajeti kubwa za misaada ya maendeleo, kulingana na IMF.