Rais wa muda mrefu nchini Uganda, Yoweri Museveni ameeleza kuwa yuko tayari kuwania muhula mwingine katika uchaguzi wa urais wa 2026.
Museveni siku ya Alhamisi alisifu nguvu zake za kimwili na ukakamavu, ambayo alisema ndiyo sababu vijana bado wanamwita kugombea muhula wa saba madarakani.
Rais alikuwa akihutubia maelfu ya wanafunzi kutoka shule mbalimbali ambao ni sehemu ya mpango wa uzalendo, katika Viwanja vya Sherehe za Kololo nchini humo.
Katika hotuba yake, Museveni aliwasihi vijana hao wasimamie maisha yao na kujilinda dhidi ya vishawishi ambavyo vitahatarisha maisha yao ya baadaye.
Alitoa mfano wake mwenyewe, ambaye katika umri wa miaka 79, bado yuko katika afya kamili.
Hii, alisema, ni kwa sababu hanywi pombe au kutumia dawa za kudhoofisha mwili.
“Sasa nitakuwa na umri wa miaka 80, lakini mnasikia mnaniuliza niendelee kuongoza nchi,” Museveni alisema.
“Hii ni kwa sababu niko fiti; Mimi si mgonjwa. Ikiwa ningekuwa mgonjwa kwenye kiti cha magurudumu hungekuwa ukinisumbua kwa kusema ‘Jaajja tova ku main’ [Babu bado una uwezo usitoke katika njia kuu]. Mnasema hivyo kwa sababu mnaona bado nina nguvu.”