Waziri wa fedha nchini Uganda, Haruna Kasolo ameripotiwa kulitaka bunge kupitisha mswada wa kuruhusu watu maskini kuwekwa katika mpango wa kucharazwa viboko na mijeledi kila wakati ili kujibidiisha katika kutafuta kazi na kuwa matajiri.
Kwa mujibu wa ripoti ya Eye Radio ya nchini humo, waziri humo alisema kwamba uongozi wa serikali ya Museveni umeweka mipango kabambe ya kuhakikisha kwamba Waganda wanatokana na umaskini na hiyo ni njia moja ya kuhakikisha azma hilo linatimia.
“Rais Museveni na serikali ya NRM tumeweka mipango kabambe ya kutokomeza umaskini tukiwa na lengo la kuhakikisha kila Mganda anakuwa tajiri, lakini kuna wengine ambao wanasuasua na kusalia kuwa maskini,” sehemu ya hotuba ya waziri huyo ilinukuliwa.
“Katika siku zijazo, serikali inaweza kupitisha sheria bungeni ambapo watu wote maskini wavivu wangepigwa mijeledi ili waweze kujifunza kufanya kazi na kuwa matajiri kwa sababu tumegundua kwamba baadhi ya Waganda wanahitaji kusukumwa katika kutwaa mali,” alisema.