Katika kutekeleza moja ya eneo la mashirikiano kati ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Wizara ya Nishati, Maji na Madini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kufanya tafiti za Jiosayansi visiwani humo, timu ya watalaam kutoka GST imeanza rasmi utafiti wa jiosayansi ili kuhakikisha kwamba Zanzibar inakuwa na ramani ya jiosayansi ambayo itawezesha kuweka mipango mahususi ya uendelezaji rasilimali zilizoko chini ya ardhi na mipango ardhi.
Akiwakaribisha wataalam wa GST katika Ofisi za Wizara ya Nishati, Maji na Madini ya Zanzibar, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Joseph John Kilangi amewashukuru watalaam hao na kuwataka kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia uzoefu wao wa masuala ya jiolojia.
Aidha, Kilangi amewahakikishia wataalam hao usalama na kupata ushirikiano kutoka Visiwa vyote vya Unguja na Pemba kwa muda wote watakaokuwa kazini.
Kwa upande wake, mtaalam kutoka GST ambaye pia ni Meneja wa Sehemu ya Jiolojia Maswi Solomon akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa GST ametoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusu umuhimu wa ramani ya jiosayansi katika visiwa vya Zanzibar ambayo haikuwepo.
Amefafanua kuwa, mbali na madini ya thamani, mafuta na gesi yaliyozoeleka pia, utafiti huo ni muhimu kuanisha maeneo yenye madini ujenzi, maeneo yenye uwezekano wa kuwa na mashimo hatarishi yaani sinkholes/caves ambayo ni miongoni mwa majanga ya asili ya jiolojia (geohazard) kutokana na visiwa hivyo kuwa na miamba yenye hali ya chokaa, maumbo ya miamba yenye kuvutia utalii (geotourism), aina ya miamba muhimu kuhifadhi maji ardhi na taarifa za kemia ya udongo.