Mvua za El Nino zinazidi kuwaathiri watu wengi nchini Kenya huku taarifa kutoka kwa idara za hali ya anga zikisema mvua hizo zitazidi kushuhudiwa kwa siku kadhaa zijazo.
Wakiwa katika makundi, wakaazi wa Kaunti ya Tana River wako kwenye harakati wakitafuta eneo la juu zaidi lililo salama, ambalo liko mbali na maeneo yaliyofurika ambayo yamefagia nyumba zao, mali zao na mifugo yao.
Si kazi rahisi au nafuu kwa watu ambao sasa wanayumbayumba kutokana na athari mbaya za mvua za El Nino.
Wakazi wa kijiji cha Bondi wanahofu kuwa maji yanaongezeka kwa kasi katika makazi yao na hivyo wanawake, watoto wanaume kufanya safari hiyo ya kujikinga huku wakiiomba serikali iwasaidie makazi kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Wakaazi hao ni miongoni mwa maelfu ya familia ambazo zimeathiriwa na mvua zinazoendelea za El Nino. Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya linasema tangu mvua kuanza kunyesha Oktoba, familia 80,518 zimeathirika, huku karibu nusu ya idadi hiyo zikihama.
Biashara, vituo vya afya, na shule pia zimeathirika huku mvua zikiendelea kunyesha sehemu mbalimbali nchini.
Idadi ya waliofariki kutokana na mvua hiyo sasa imefikia 61, huku watu 235 wameripotiwa kujeruhiwa na wengine wanane wameorodheshwa kama hawajulikani walipo.