Ismail Haniyeh ameliambia shirika la habari la Reuters siku ya Jumanne kwamba Palestina iko karibu kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na utawala wa Kizayuni.
Ismail Haniyeh, Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu Hamas amesema katika taarifa iliyotumwa kwa Reuters na msaidizi wake kuwa maafisa wa Hamas wanakaribia kufikia makubaliano ya kusitisha vita na Israel, na majibu yetu yamefikishwa kwa wapatanishi wa Qatar.
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la habari la Palestina la Shahab, Ezzat al-Rashq, mmoja wa viongozi wa Hamas pia amesema: Tumeshuhudia maendeleo makubwa katika mazungumzo na tunakaribia usitishaji vita, makubaliano yote yamechukuliwa kwa mujibu wa matakwa ya wanamuqawama.
Amesema kwamba hataki kutoa maelezo zaidi kuhusu mazungumzo hayo na kuongeza: Ndugu zetu wa Qatar na Misri watatangaza karibuni maelezo ya makubaliano hayo, na usitishaji mapigano.
Huku akisisitiza kuwa upande wa Israel hususan Netanyahu unachelewesha njia ya mapatano, amesema: ‘Wanamuqawama katika medani ya vita na siasa wako pamoja na mapatano haya yanajumuisha makundi yote. Waisraeli wanajaribu kukandamiza makundi ya wanaharakati wa Kipalestina na kuendeleza mazungumzo huku wakidumisha uvamizi wao, lakini jambo hilo halitatokea.’