Mamlaka ya masoko ya mitaji na dhamana (CMSA) imeitaka jamii kujihadhari na upatu haramu kwani ni hatari kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Meneja uhusiano wa CMSA Charles Shirima ameyasema hayo jijini Arusha wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya wiki ya huduma za fedha kitaifa ambapo amesema jamii ijihadhari na matapeli wanaoahidi watu kuvuna pesa nyingi kirahisi hivyo waepuke kupoteza pesa ya jasho lao kupitia upatu haramu.
“Kutokana na hali hiyo watanzania wanapaswa kujiinga kwenye masoko ya mitaji kwani ni sehemu ya mfumo wa sekta ya fedha unaowezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo ya muda mrefu yaani mwaka mmoja,” amesema
Amesema fedha za maendeleo hupatikani kwa kuuza hisa za kampuni, hatifungani za kampuni na vipande katika uwekezaji wa pamoja.
Mchambuzi fedha mwandamizi wa CMCA, Witness Gowelle amesema kupitia maadhimisho hayo wametoa elimu kwa wajasiriamali mbalimbali ili kuwajengea uwezo zaidi.
“Elimu mbalimbali tuliyotoa kwa wajasiriamali watanufaika nao kupitia masoko ya mitaji ili kujiepusha na upatu haramu,” amesema Gowelle.
Maadhimisho ya wiki ya huduma za fedha kitaifa kupitia kauli mbiu ya elimu ya fedha, msingi wa maendeleo ya uchumi, yanafanyika jijini Arusha, kwa siku sita kuanzia Novemba 20 hadi 26 mwaka huu.