Idadi ya waliofariki kutokana na mafuriko nchini Somalia inakaribia 100, huku takriban watu milioni mbili wakiathirika, baraza la mawaziri la nchi hiyo limesema siku ya Alhamis ya wiki hii.
Somalia, kama nchi nyingine katika Pembe ya Afrika, inakabiliwa na mvua kubwa na mafuriko, wakati huu ikiwa imetoka kushuhudia hali mbaya kutokana na ukame uliowaweka mamilioni ya raia kwenye hatari ya kufa kutokana na baa la njaa.
Serikali mapema mwezi huu, ilitangaza hali ya hatari kutokana na mafuriko, ambayo yamesababisha watu zaidi ya laki 7 kupoteza makazi, mashamba na miundombinu mingine.
Mvua zinazoendelea kunyesha nchini humo zinahusishwa na hali ya hewa ya El Nino, ambayo inatarajiwa kudumu hadi angalau mwezi April mwakani.
Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kutoa misaada ya kibinadamu OCHA, mamia ya watu wamefariki pia katika nchi za Ethiopia na Kenya, mashirika ya misaada yakionya kuwa huenda hali ikawa mbaya zaidi.