Vladimir Putin ameripotiwa kuwasamehe wanaume wawili wa Urusi waliopatikana na hatia ya kula nyama za watu baada ya kupelekwa mstari wa mbele katika vita na Ukraine.
Mmoja wa watu hao, Denis Gorin, aliandikishwa katika kampuni ya kijeshi ya kibinafsi baada ya kutia saini mkataba na wizara ya ulinzi ya Urusi lakini anajulikana kuwa alihukumiwa mara tatu kwa mauaji ya watu wanne kati ya 2003 na 2022.
Pia alipatikana na hatia ya kula mabaki ya wahasiriwa wake pamoja na kaka yake, iliripoti Sibir Realii, chombo cha habari kilichounganishwa na Radio Free Europe.
Mwanamume mwingine, Nikolai Ogolobyak, alipatikana na hatia ya mauaji ya kitamaduni, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Urusi.
Alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela mwaka wa 2019 kwa kuwaua vijana wanne na kisha kula mabaki yao.
Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 33 aliripotiwa kusamehewa wiki hii na rais wa Urusi kwa kupigana katika uvamizi wa Ukraine.