Hakimu mkuu nchini Uganda aliyekamatwa kwa tuhuma za ufisadi alizua kizaazaa katika mahakama ya mjini Kampala baada ya kuanza kupiga mayowe akilia na kujigaragaza sakafuni.
Kwa mujibu wa jarida la Independent, hakimu mkuu huyo, Sylvia Nvanungi, ni wa mahakama ya Mitooma na baada ya kisanga hicho, aliwekwa kwenye rumande na mwenzake, Wakili wa Serikali Mkazi wa Sembabule, Jacqueline Bako, kwa tuhuma za rushwa.
Wawili hao walifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Kupambana na Ufisadi Joan Aciro ambaye aliwashtaki kwa makosa manane ya ufisadi.
Bako alihusishwa na mashtaka yote, huku Nvanungi akihusishwa katika shtaka moja. Makosa haya yanadaiwa kutokea wakati Nvanungi akiwa Hakimu Mkuu wa Sembabule mapema mwaka huu.
Mahakama ilisikiza kuwa Aprili 2023, wakiwa kwenye nyadhifa za umma, wawili hao wanadaiwa kuomba kulipwa Shilingi milioni 2.5 za Uganda kutoka kwa jamaa za washukiwa.
Mshtakiwa alikana mashitaka hayo na kuomba apewe dhamana. Mahakama ilikataa ombi lao kwa sababu ya ukosefu wa wadhamini wa kuaminika.