Tawi la kijeshi la Hamas limetangaza Jumapili hii kifo cha kamanda wa kijeshi wa Brigedi ya Kaskazini ya Gaza na maafisa wengine watatu, wakati wa shambulio la Israel kwenye ardhi ya Palestina.
Ahmed al-Ghandour alikuwa mjumbe wa Baraza la Kijeshi la Hamas na alichukuliwa kuwa “gaidi” na mamlaka ya Marekani tangu mwaka 2017, hasa kwa jukumu lake katika mashambulizi dhidi ya jeshi la Israel mwaka 2006 katika kivuko cha Kerem Shalom, kati ya Israel na Ukanda wa Gaza, kusini mwa Palestina.
Akiwa analengwa kwa muda mrefu na jeshi la Israel, alipoteza watoto wake wawili katika mashambulizi kabla ya mashambulizi ya sasa. Miongoni mwa maafisa wengine watatu waliotajwa kwenye taarifa kwa vyombo vya habari ni Ayman Siam, aliyewasilishwa kama mkuu wa vitengo vya kurusha roketi.
“Tunaapa mbele ya Mwenyezi Mungu kwamba tutaendelea na njia yao na kwamba damu yao itakuwa nuru kwa mujahidina na moto dhidi ya wavamizi,” Brigedi za al-Qassam zimzsema katika taarifa yao.
Hamas mara chache huwasiliana kuhusu vifo vya wapiganaji wake. Hata hivyo, katikati ya mwezi Oktoba, kundi la Hamas lilitangaza kifo cha Aymane Nofal, kamanda wa Kikosi cha Al-Qassam, katika shambulio la jeshi la Israel kwenye kambi ya wakimbizi ya Bureij katikati mwa Palestina.