Mahakama ya Korea Kusini imemhukumu mwanaume wa miaka 68 kifungo cha miezi 14 jela kwa kusifu eneo la Kaskazini katika shairi.
Lee Yoon-seop alitetea muungano katika shairi lake ambalo lilichapishwa kwenye vyombo vya habari vya serikali ya Kaskazini mnamo 2016, ripoti ya vyombo vya habari vya Korea Kusini.
Aliandika kwamba iwapo Korea hizo mbili zingeungana chini ya mfumo wa ujamaa wa Pyongyang, watu wangepata nyumba, huduma za afya na elimu bure.
Alipatikana na hatia chini ya sheria inayokataza kusifiwa hadharani kwa Korea Kaskazini. Katika shairi hilo lenye jina, Njia za Kuungana, Lee pia alisema kuwa katika Korea iliyoungana, watu wachache watajiua au kuishi kwa madeni.
Shairi hilo lilikuwa la kwanza kwenye shindano la ushairi Kaskazini mnamo Novemba mwaka 2016.
Lee alifungwa jela kwa miezi 10 huko nyuma kwa kosa kama hilo, iliripoti Korea Herald.
Katika uamuzi wake wa Jumatatu, mahakama ya Seoul ilisema “aliendelea kuzalisha na kusambaza kiasi kikubwa cha propaganda ambazo ziliitukuza na kuisifu Kaskazini,” Korea Herald ilisema.