Nchi ya Uganda inajiandaa kukopa dolla millioni 150, kutoka kwa benki ya China ya (Exim), kufanikisha miradi yake baada ya benki ya dunia kusitisha misaada yake kwa nchi hiyo kutokana na sheria kali dhidi ya wapenzi wa jinsia moja.
Uganda inakopa pesa hizo kwa benki ya EXIM, ili kuimarisha miundo mbinu yake ya mitandao, wizara ya fedha nchini humo imetangaza, wakati huu Uganda ikiendelea kutegemea mikopo kujiendeleza.
Wizara ya feha nchini humo sasa ikilitaka bunge, kuidhinisha serikali kuomba mkopo huo kutoka China.
Benki ya Dunia ambayo ndiyo ilikuwa mshirika mkuu wa Uganda na pia mkopeshaji wake, ilisitisha uhusiano na taifa hilo la Afrika mashariki baada ya rais Yoweri Museveni, kuidhinisha sheria kali dhidi ya wapenzi wa jinsia moja ikiwemo kuwaadhibu na hukumu ya kifo, sheria ambao pia imekashifiwa na mataifa kadhaa ikiwemo Marekani na Umoja wa Ulaya.