Afrika Kusini, nchi iliyo na visa vingi zaidi vya VVU ulimwenguni, imerekodi kupungua kwa mara ya kwanza kwa idadi ya watu walioambukizwa virusi hivyo, kulingana na utafiti uliochapishwa Jumatatu.
Kulingana na Baraza la Utafiti wa Sayansi ya Binadamu (HSRC), taasisi ya utafiti wa umma ya Afrika Kusini, ambayo imefanya uchunguzi wa watu 76,000, asilimia ya Waafrika Kusini walio na virusi vya Ukimwi (VVU) vinavyosababisha UKIMWI ilipungua kwa 1.3% kati ya mwaka 2017 na 2022, kutoka 14% hadi 12.7% ya raia.
Hivyo, mwaka 2022 baadhi ya Waafrika Kusini milioni 7.8 kati ya wakazi milioni 62 walikuwa na virusi hivyo ikilinganishwa na milioni 7.9 mwaka 2017, tarehe ya uchunguzi wa mwisho. Sababu za kupungua kwa ugonjwa huo ni nyingi, amesema Khangelani Zuma, mkurugenzi wa HSRC na mtafiti mkuu wa utafiti huo.
Licha ya kupungua kwa idadi ya watu walio na virusi vya Ukimwi katika majimbo yote, mashariki mwa nchi na hasa eneo la Wazulu limesalia kuathirika zaidi. Jamii ya watu weusi ndio walioathirika zaidi.
Bw Zuma pia amebainisha kuwa watu wanaishi kwa muda mrefu na VVU kuliko hapo awali, kutokana na matumizi makubwa ya tiba ya kurefusha maisha (ART) ambayo imebadilisha kwa kiasi kikubwa mtazamo wa watu wenye UKIMWI/VVU. Hata hivyo, Afŕika Kusini pekee bado inawakilisha theluthi moja ya wagonjwa barani Afŕika, na zaidi ya vifo 85,000 vya UKIMWI kila mwaka katika miaka ya hivi majuzi.