Mahakama ya kikatiba nchini Uganda, imetenga tarehe 11 ya mwezi ujao kuanza kutoa uamuzi katika mapingamizi manne kuhusu uhalali wa sheria tata kuhusu ushoga iliyopitishwa na Serikali mwezi Mei mwaka huu.
Tangazo hili la Mahakama limekuja baada ya waombaji kukubaliana kuweka mapingamizi yao kama shauri moja, baada ya maombi ya mwanasheria mkuu wa Serikali.
Kwa mujibu wa mapingamizi yaliyowasilishwa na karibu mashirika 19, wanasema sheria hiyo ilipitishwa kinyume na katiba ya Uganda ambayo inazungumzia uhuru wa watu kujiamulia.
Hata hivyo licha ya ukosolewaji mkubwa, serikali imeendelea kutetea sheria hiyo, ikisema inalenga kulinda maadili na utamaduni wa Uganda na haiendi kinyume na haki za binadamu.
Tangu kupitishwa kwa sheria hiyo, mashirika kadhaa ya misaada ikiwemo USAID, Marekani na benki ya dunia yalitangaza kusitisha misaada yao kwa Uganda.