Rapa na mtendaji mkuu wa muziki kutoka Marekani, Sean Combs, almaarufu Diddy, amejiuzulu kama mwenyekiti wa kampuni ya habari ya Revolt TV.
Kampuni hiyo, katika taarifa iliyotolewa kwenye ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumanne, ilieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu ili kuwezesha Revolt kuzingatia dhamira yake.
Kulingana na taarifa hiyo: “Sean Combs amejiuzulu kutoka nafasi yake kama mwenyekiti , kulenga dhamira yetu ya kuunda maudhui yenye maana kwa utamaduni na kukuza sauti za watu wote Weusi nchini kote na ugenini wa Afrika.
Revolt ilianzishwa na Diddy pamoja na afisa mkuu wa vyombo vya habari Andy Schuon mwaka wa 2013, kwa lengo la kuonyesha utamaduni wa hip-hop na sauti za watu weusi nchini Marekani.
Katika siku za hivi karibuni, Combs amekuwa katika kesi kadhaa za kisheria na madai ya unyanyasaji wa kijinsia.
Mpenzi wake wa zamani, Casandra Ventura, mapema mwezi Novemba alimshtaki mwimbaji huyo kwa kumnyanyasa kimwili na kingono katika uhusiano wao wa muongo mzima.
Wiki moja baada ya kesi ya kwanza, Joi Dickerson-Neal pia alimshtaki rapper huyo, akidai kwamba alimnywesha dawa za kulevya na kumbaka mwaka wa 1991.
Kesi ya tatu iliwasilishwa na mlalamikaji aliyejulikana tu kama Jane Doe, ambaye alidai kuwa Diddy na msanii wa R&B Aaron Hall walichukua zamu kumnyanyasa yeye na wanawake wengine katika nyumba ya mwimbaji huyo mapema miaka ya 1990.
Diddy alikuwa amekanusha madai hayo yote, akiyataja kama “madai ya kubuni” na majaribio ya “kunyakua pesa.”