Kiongozi mkuu wa benki kuu ya Ethiopia alisema taifa hilo la Pembe ya Afrika ambalo limekabiliwa na uhaba wa fedha limepata makubaliano ya msamaha wa deni ya dola bilioni 1.5 na wakopeshaji.
Hatua hiyo inaipunguzia Ethiopia mzigo wa kifedha kwa muda inapotafuta mpango mpana wa ufadhili.
Makubaliano hayo yalitangazwa Jumatano na Gavana wa Benki ya Kitaifa ya Ethiopia Mamo Mihretu na kuthibitishwa katika taarifa ya Klabu ya Paris ya mataifa ya wadai siku ya Alhamisi ambayo ilieleza kuwa ni “mafanikio muhimu”.
“Tumeweza kufikia usitishaji wa huduma ya deni kwa muda na kwa hivyo kuweza kuokoa karibu dola bilioni 1.5 ambazo zingetumika kulipa deni,” Mamo aliiambia kamati ya bunge.
Uchumi wa Ethiopia umekumbwa na mzozo wa miaka miwili katika eneo la kaskazini la Tigray uliomalizika kwa makubaliano ya amani mwezi Novemba mwaka jana.