Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa amewataka watumishi wa sekta ya ardhi kubadilika na kufanya kazi kwa weledi na kuwatumikia wananchi kwa kuzingatia taaluma zao na kama hawawezi kwenda na kasi yake hatopenda waendelee kuwa watumishi wa Wizara hiyo.
Amesema hayo leo Jumatatu Desemba 4, 2023 wakati akizungumza na baadhi ya viongozi, maafisa, watumishi wa idara ya ardhi pamoja na wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Shinyanga wakiwemo wakuu wa Wilaya na wabunge kutoka kwenye majimbo ya Mkoa wa Shinyanga.
Waziri Silaa amesema wale wote ambao wako tayari kufanya kazi na yeye basi wabadilike ili kusimamia kazi kikamilifu na ambao wanaona watashindwa kwenda na kasi yake basi wajiengue mapema.
Kwa upande wake kamishna msaidizi wa ardhi Mkoa wa Shinyanga Leo Komba amesema Mkoa wa Shinyanga umefanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na wizara huku akiahidi kuendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinazojitokeza.
Waziri Mhe. Silaa amefika Mkoani Shinyanga kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa maelekezo ya baraza la mawaziri kuhusu utatuzi wa migogoro ya ardhi.