Katibu mkuu wa wizara ya nishati mhandisi Felchesmi Mramba ameongoza ujumbe wa Wataalam wa Wizara na Taasisi zilizo chini yake, katika Mkutano wa 28 wa Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) ulioanza rasmi Novemba 30 hadi unatarajiwa kuisha Desemba 12, 2023.
Katika Mkutano huo Wizara ya Nishati na Taasisi zake imeandaa na kufanikisha uzinduzi wa programu ya Nishati Safi ya Kupikia kwa Wanawake wa Afrika (AWCCSP) uliofanywa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kushuhudiwa na Watu Mashuhuri wakiwemo Marais wa nchi mbalimbali
Wizara inaratibu pia mikutano na mawasilisho mbalimbali kwa lengo la kutangaza fursa za Uwekezaji katika miradi ya Nishati Jadidifu inayolenga kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa, kuelezea jitihada zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia Sekta ya Nishati, kuimarisha ushirikiano baina ya Wizara na wadau wa Nishati pamoja na kupata uzoefu kutoka nchi zilizoendelea katika masuala ya nishati