Mwanzoni mwa wiki hii, serikali ya Marekani ilipanua sera za kuzuia visa kwa maafisa wa serikali ya Uganda ili kuwajumuisha wale inaowaamini kuwa wanahusika kwenye kudhoofisha demokrasia na kukandamiza makundi ya LGBTQ+ nchini Uganda huku pia ikitangaza sera mpya ya kuzuia visa kwa maafisa wanaopinga demokrasia nchini Zimbabwe.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alitangaza kuwekwa kwa vikwazo vya visa na akataja, miongoni mwa mengine, kutengwa kwa makundi kama vile jumuiya ya LGBTQ nchini Uganda na watetezi wa mashirika ya kiraia nchini Zimbabwe.
Sheria dhidi ya kundi la LGBTQ nchini Uganda inachukuliwa kama moja ya sheria kali zaidi duniani, ilitungwa mwezi Mei ikiwa na adhabu ya kifo kwa makosa ya “ushoga uliokithiri,” kosa ambalo ni pamoja na kusambaza VVU kwa njia ya mashoga. Mwezi Juni, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliweka vikwazo vya visa kwa maafisa wa Uganda baada ya kupitishwa kwa sheria hiyo.
Wizara ya Mambo ya Nje pia hapo awali iliweka vizuizi vya visa kwa maafisa wa Uganda kufuatia uchaguzi wa mwaka 2021 nchini humo, ambao iliutaja kuwa ‘una dosari.’