Madaktari wenye ujuzi wa kufanya tathmini ya ulemavu unaotokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi (Impairment Assessment of Occupational Accidents and Diseases) wamefikia 1,722 Nchi nzima, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, amesema.
Mhe. Babu amesema hayo mjini Moshi, Desemba 5, 2023, wakati akifungua mafunzo ya ya kuwajengea uelewa madaktari na watoa huduma za afya, kufanya tathmini ya ulemavu unaotokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi (Impairment Assessment of Occupational Accidents and Diseases).
“Ili Mfuko uweze kufikia azma ya Serikali ya kuhakikisha wafanyakazi wanaopata ulemavu au magonjwa yatokanayo na kazi, wanapata fidia stahiki na kwa wakati, lazima wawepo madaktari wenye ujuzi wa kufanya kazi hiyo.” Amefafanua.
Alisema WCF, ambayo ilianza kutekeleza majukumu yake miaka 8 iliyopita, ilianza zoezi hili la kutoa mafunzo katika mwaka wa fedha 2015/16 mpaka sasa.
“WCF inatuhakikishia kuwa itaendelea kutoa mafunzo haya kwa wadau wengi zaidi ili kuweza kutimiza nia njema ya Serikali iliyopelekea kuundwa kwa taasisi hii muhimu.” Amesema Mhe. Babu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma amebainisha kuwa, mafunzo hayo yamewaleta pamoja madaktari 100 kutoka hospitali za umma na binafsi, kwa ngazi zote, kuanzia vituo vya afya hadi hospitali za rufaa za kanda.
“Awali uelimishaji wa aina hii ulianzia ngazi ya hospitali za Wilaya, hata hivyo, ili kuhakikisha Mfuko unaendana na kasi ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kufungua Nchi, ambapo uwekezaji umeongezeka katika maeneo mbalimbali, na si tumeona tupanue wigo wa kuelimisha wataalamu wetu kuanzia ngazi ya vituo vya afya.” Amefafanua Dkt. Mduma na kuongeza..hii itasaidia kusogeza huduma karibu zaidi kwa walengwa,” amefafanua.
Akizungumzia mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini, Dkt. Abdulsalaam Omar, amesema, baadhi ya mambo ambayo madaktari hao wamejifunza ni pamoja na Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi [Sura 263 marejeo ya mwaka 2015], Mchakato wa Uwasilishaji Madai, Dhana ya Usalama na Afya mahali pa Kazi, Jinsi ya Kudhibiti Vihatarishi sehemu za kazi, Jinsi ya kufanya Tathmini ya Vihatarishi, Kuchunguza magonjwa yatokanayo na kazi, Udhibiti wa Ajali na Magonjwa mahali pa kazi, jinsi ya kufanya Tathmini ya Ulemavu, Jinsi ya kufanya Tathmini ya Magonjwa yatokanayo na kazi na Mafao yatolewayo na Mfuko
Wakitoa maoni yao kuhusu mafunzo hayo, baadhi ya washiriki walisema, yamewajengea uelewa mzuri wa namna ya kumuhudumia mfanyakazi aliyeumia au kuugua kutokana na kazi lakini pia kutambua kuwa hata wao pia huduma za WCF zinawahusu.
Dkt. Cresencia Edmond, kutoka Hospitali ya St. Elizabeth, amesema, amefurahi kupata ujuzi mpya kuhusiana na kazi zake lakini hata yeye binafsi kama mfanyakazi.
“Elimu ya kujiepusha na vihatarishi vinavyoweza kupelekea mtu kuathirika na magonjwa au ajali zitokanazo na kazi, mfano maumivu ya mgongo (back pain) yanayosababishwa na ukaaji au matumizi ya viti visivyofaa kiafya.” Amesema Dkt. Edmond.
Naye Dkt. AzariaSimon mshiriki kutoka hospitali ya Haidom, yeye amesema amefurahishwa na Dhima (Mission) ya Mfuko ambayo ni kupunguza athari za kijamii na kiuchumi za majanga yatokanayo na kazi kwa wafanyakazi, familia zao na waajiri kwa kutoa fidia stahiki, kwa usawa, uendelevu na ufanisi.
“Hiyo ndiyo nimeipendelea pamoja na mambo mengine kama vile jinsi ya kutoa taarifa kupitia mifumo, mtu (mfanyakazi) anapopatwa na matatizo akiwa kazini.” Amefafanua.