KATIKA kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kuimarisha shughuli za kihandisi nchini, Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imetoa wito kwa sekta ya umma kuweka mpango madhubuti wa usimamizi wa miradi ya ujenzi kuanza hatua za awali za usanifu, ujenzi, kukamilika hadi kutumika kwake ili miradi hiyo iweze kudumu kwa muda mrefu.
Pia imetoa ushauri kwamba kuwepo na uwajibikaji kwa wahandisi pindi wanaposhindwa kusimamia misingi ya taaluma yao katika masuala hayo ya ujenzi ili kuimarisha shughuli za kihandisi kwa upande wa sekta ya umma.
Wito huo umetolewa juzi na Mhandisi wa GGML anayedhibiti ubora na viwango vya miradi, Maftah Seif wakati akichangia mada katika Kongamano la Kitaifa la 32 la Taasisi ya Wahandisi Tanzania lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Arusha (AICC).
Seif alikuwa anachangia mada kuhusu sababu za kitengo cha matengenezo kwenye miradi inayohusu ujenzi wa mitambo na majengo katika sekta ya umma kudorora ilihali kwenye sekta binafsi inadumu kwa muda mrefu.
“Tunashauri kwanza kuwe na mpango mzuri kuanzia mradi unapoandaliwa, unapojengwa, unapomalizika na kwenda kwenye hatua za operesheni (matumizi) kwamba kuwe na namna kuusimamia.
“Kwa mfano mradi unapojengwa ukikamilika lazima kuwe na gharama za kuuendesha kwa sababu mradi unaishi hivyo lazima kuwe na gharama za matengenezo.
“GGML tunaamini mradi hauwezi kufa bila kujua ndio maana pia tunatoa ushauri kwenye maeneo makubwa mawili kwani dunia imehama kutoka utamaduni wa kawaida na kuwa na wabobezi wanaojua kutumia teknolojia mbalimbali,” amesema.
Aidha, Seif ambaye alikuwa mmoja wa wahandisi 16 walioshiriki kongamano hilo kutoka GGML, alisema ili kufanikisha mabadiliko hayo kwa upande wa sekta ya umma, lazima kuwe na rasilimali watu.
“Lakini pia kuwe na uwajibikaji hasa kwetu wahandisi, tuondoke kwenye utamaduni wa kufanya kazi kwa mazoea, kuwe na idara inayompima na kumbana mhandisi husika anapokiuka vigezo vya mradi badala ya kuubana uongozi wa juu ambao hauhusiki moja kwa moja,” alisema.
Awali akizungumza katika kongamano hilo, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa aliiagiza Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kushirikiana na Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET) kuweka utaratibu endelevu wa kuwajengea uwezo wahandisi ili waweze kuendana na mabadiliko ya teknolojia.
Akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Bashungwa alisema mhandisi ni mwanafunzi maisha yake yote hivyo aliwaagiza ERB wakiungwa mkono na IET kuweka mpango maalumu wa kuwapatia ujuzi wahandisi walioko kazini kwa kutumia miradi iliyopo.
Bashungwa pia aliitaka Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kupitia upya vigezo vya usajili wa wahandisi kwa kufungua milango na kuondoa vikwazo visivyo vya lazima katika usajili.
“Idadi ya wahandisi mahiri inatakiwa kuwa muhandisi mmoja kati ya wananchi 5,000, kwa hesabu za haraka, tunatakiwa kuwa na wahandisi mahiri zaidi ya 12,000 lakini nimeambiwa wahandisi washauri waelekezi ni chini ya 500,” alisema.
Aidha, Bashungwa alisema azma ya Serikali ni kujenga uchumi ulio imara ndio maana imejieelekeza kwa kiwango kikubwa kujenga uwezo, juhudi, maarifa, weledi, nidhamu, umakini na ufanisi kwa wataalam hao.
Pamoja na mambo mengine Bashungwa aliipongeza GGML na kuipatia zawadi ya cheti kwa kutambua mchango wa kampuni hiyo katika kuwezesha kongamano hilo pamoja na ushiriki wake.