Jeshi la Polisi nchini limesema kuwa litawafungia leseni madereva wote wanaosababisha ajali huku likibainisha kuwa katika siku za hivi karibuni kumeendelea kujitokeza ajali za barabarani zilizosababisha vifo na majeruhi kwa watanzania ambapo. Chunguzi zinapofanyika zinaonyesha chanzo ni uzembe wa madereva wanaoendesha magari hayo.
Akitoa taarifa hiyo leo disemba 06,2023 msemaji wa Jeshi la Polisi nchini kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi SACP David Misime amesema kuwa chanzo cha ajali hizo ni Uzembe pamoja na mwendo kasi na kupita magari mengine (overtake) bila kuchukua tahadhari maeneo ambayo alama za barabarani zimekataza.
Ameendelea kusema kuwa pamoja na uzembe huo unaofanywa na baadhi ya madereva, wa magari hayo kumekuwa na maneno ya kuiaminisha jamii kuwa mwisho wa mwaka ajali zinakuwa nyingi, jambo ambalo si sahihi huku akiwataka madereva kuondoa dhana hiyo ambayo inapotosha umma wa Tanzania.
SACP Misime amebainisha kuwa kufika kwa mwisho wa mwaka hakujabadili sheria za usalama barabarani wala alama za makatazo na ishara za barabarani.ambapo amewataka madereva kuzifuata sheria hizo ili kuepuka ajali za barabarani.
Aidha Msemaji wa Jeshi hilo amewambia madereva na wananchi kuwa kinachobadilika ni tabia za baadhi ya madereva wa vyombo vya moto wasiotaka kuzingatia sheria za usalama barabarani na kufuata alama za makatazo na zile za ishara za barabarani na matokeo yake wanasababisha ajali.
Sambamba na hilo amesema Jeshi la Polisi nchini linapenda kusisitiza, kuwa kwa watumiaji wa barabara wakiwemo watembea kwa miguu, wasukuma mikokoteni, waendesha baiskeli na waendesha vyombo vya moto wazingatie sheria za usalama barabarani huku akiwaomba Viongozi wa serikali kuwaonya madereva wao pale wanapokiuka sheria za usalama barabarani.
Msemaji wa Jeshi hilo amewambia waandishi wa Habari kuwa Jeshi la Polisi nchini litaendelea kuchukua hatua kali za kisheria kuwafutaia leseni zao ikiwa ni Pamoja na kuwafikisha mahakamani kwa makosa hayo ya usalama barabarani.