Nyota maarufu wa reggaeton Ramón Ayala, almaarufu Daddy Yankee, amestaafu rasmi muziki.
Mwimbaji na rapper wa Puerto Rican alitangaza haya kwenye jukwaa wakati wa siku ya mwisho ya ziara yake ya kuaga, La Meta, huko Puerto Rico mwishoni mwa wiki.
Alisema sasa anatumai “kuiinjilisha dunia” na kuishi kwa ajili ya Yesu.
Katika ujumbe wa video uliosambazwa kupitia ukurasa wake wa Instagram, ‘The King Of Reggaeton’ alisema kuwa sehemu yake alihisi tupu na amekuwa akijaribu kuziba pengo maishani mwake kwa muda mrefu ambalo hakuna mtu angeweza kuliziba.
Katika ujumbe wake, mwimbaji ‘Despacito’ alitaja mstari wa Biblia; “Niliweza kuzunguka ulimwengu kwa miaka mingi nikishinda tuzo nyingi, makofi na sifa, lakini nilitambua jambo ambalo Biblia husema, ‘yafaa nini mtu kuupata ulimwengu wote ikiwa anaipoteza nafsi yake?’”
Aliongeza: “Hadithi moja imekwisha na hadithi mpya itaanza, mwanzo mpya.”
Daddy Yankee alianza kazi yake mnamo 1994 na anachukuliwa kuwa mmoja wa waanzilishi wa aina ya reggaeton.
Alistaafu akiwa na umri wa miaka 46.