Waendesha mashtaka wa kupinga matumizi ya dawa za kusisimua misuli nchini Italia waliomba kufungiwa kwa miaka minne kiungo wa Juventus Paul Pogba siku ya Alhamisi baada ya mshindi huyo wa Kombe la Dunia 2018 kukutwa na testosterone.
Pogba aliamua kutofanya makubaliano na wakala wa kupambana na dawa za kusisimua misuli nchini Italia, kumaanisha kuwa kesi hiyo itasikilizwa mbele ya mahakama ya nchi hiyo inayokabiliana na matumizi ya dawa hizo.
Marufuku ya miaka minne ni ya kawaida chini ya Kanuni ya Ulimwenguni ya Kuzuia Matumizi ya Madawa ya Kulevya lakini inaweza kupunguzwa katika hali ambapo mwanariadha anaweza kuthibitisha kuwa dawa hiyo haikukusudiwa, ikiwa kipimo chanya kilitokana na uchafuzi au ikiwa watatoa “msaada mkubwa” kusaidia wachunguzi.
Tangu kutangazwa kwa kuwa amepatikana na hatia hiyo, Pogba hawezi tena kufanya mazoezi na Juventus Turin. Klabu ya Piedmont, ambapo alirejea mnamo mwezi wa Julai 2022 baada ya misimu sita katika Manchester United, imesitisha malipo ya mshahara wake unaokadiriwa kuwa euro milioni 8 kwa mwaka hadi mwaka 2026.
Suala hili la matumizi ya dawa za kusisimua misuli ni matokeo ya mwisho ya mwaka mmoja na nusu mbaya kwa Pogba.
Akiwa uwanjani, alicheza mechi kumi pekee akiwa na Juve msimu uliopita, kutokana na jeraha la meniscus kwenye goti lake la kulia, ambalo aliishia kufanyiwa upasuaji mwezi Septemba. Imechelewa mno kwa mfungaji katika fainali ya Kombe la Dunia 2018 kuweza kucheza Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar.