Imetajwa kuwa idadi kubwa ya watu barani Afrika – karibu asilimia 78, au zaidi ya watu bilioni moja – bado hawawezi kumudu lishe bora, ikilinganishwa na asilimia 42 katika kiwango cha kimataifa, na idadi inaongezeka.
Haya yamo kwenye ripoti iliyozinduliwa Alhamisi huko Johannesburg, Afrika Kusini na mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa lile la chakula na kilimo FAO, na la mpango wa chakula duniani WFP, Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) na Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Afrika (ECA).
Aidha ripoti hiyo inaonyesha kwamba mnamo mwaka 2022, takriban Waafrika milioni 342 walikuwa “na uhaba wa chakula,” hiyo iliwakilisha 38% ya watu milioni 735 wenye njaa kote ulimwenguni.
Ripoti hiyo imesema miongoni mwa walioathiŕika zaidi na mgogoŕo wa chakula baŕani Afŕika ni watoto walio chini ya umŕi wa miaka 5, asilimia 30 kati yao wakiwa wamedumaa kwa sababu ya utapiamlo.
Ripoti hiyo ya uhakika wa chakula na lishe kanda ya Afrika 2023 imeangazia takwimu za kutisha za ukosefu wa chakula na utapiamlo ambazo zinasisitiza haja ya haraka ya hatua za kina kuchukuliwa ili kuepusha mgogoro mkubwa. Aidha ripoti hiyo imeonya kwamba “mamilioni ya watu wanatarajiwa kuwa katika hatari ya njaa katika siku za usoni kote Afrika.”
Huku idadi ya vijana ikitarajiwa kuongezeka maradufu ifikapo mwaka 2050, Afrika ndilo eneo pekee linalokuwa kwa kasi ambapo watu wanazidi kuwa maskini. Licha ya utajiri wake wa maliasili, Afrika iko mbali na kutimiza ahadi yake ya kumaliza njaa na aina zote za utapiamlo ifikapo 2025.