Erik ten Hag alisema alionywa kuchukua “kazi isiyowezekana ya umeneja wa Manchester United lakini akakiri asingeweza kupinga changamoto hiyo Old Trafford.
Mholanzi huyo, ambaye aliondoka Ajax na kuchukua mikoba ya United mnamo 2022, alimaliza ukame wa klabu hiyo uliodumu kwa miaka sita msimu uliopita lakini amekuwa kwenye shinikizo kubwa katika kampeni yake ya pili.
“Kila mtu alikuwa akiniambia ‘Huwezi kufaulu katika kazi hiyo’,” alisema kocha huyo mwenye umri wa miaka 53. “Walisema haiwezekani. Mimi? Nilitaka changamoto.”
United iliifunga Newcastle katika fainali ya Kombe la Ligi mwezi Februari na kumaliza nafasi ya tatu kwenye Ligi ya Premia 2022/23.
Lakini msimu huu tayari iko nje ya Kombe la Ligi, ikiwa nyuma ya kinara wa Ligi Kuu, Arsenal kwa pointi tisa na inakabiliwa na aibu ya kuondolewa katika hatua ya makundi kutoka kwa Ligi ya Mabingwa.
Tangu Alex Ferguson alipostaafu mwaka wa 2013, makocha sita wamejaribu na kushindwa kuirejesha United kileleni mwa soka ya Uingereza — David Moyes, Louis van Gaal, Jose Mourinho, Ole Gunnar Solskjaer na Ralf Rangnick.
“Nilijua haingekuwa rahisi, lakini ilikuwa klabu kubwa yenye mashabiki wengi,” alisema Ten Hag.
“Watu wanaipenda Man Utd, au wanapingana na Man Utd. Napenda vilabu kama hivi. Ajax ilikuwa hivi.”