Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) kimesema kuwa kinajivunia mafanikio makubwa kiutendaji yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka huu na kuifanya TUGHE kuwa Chama kinachosimamia vema maslahi ya wafanyakazi nchini
Akifungua Mkutano wa Baraza Kuu TUGHE 2023, Mwenyekiti wa TUGHE Taifa Cde, Joel George Kaminyoge amesema kuwa TUGHE inajivunia kuona Chama kimeendelea kuwasemea wanachama wake katika maeneo mbalimbali na pia akatumia nafasi hiyo kuwataka Wajumbe wa Baraza Kuu kushiriki kikamilifu katika Mkutano huo na wajione ni chachu ya kuleta mabadiliko yatakayokijenga Chama cha TUGHE.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Hery Mkunda amesema kuwa Baraza Kuu ni moja ya Vikao vya Kikatiba ambapo Wajumbe hukutana kufanya tathmini ya Utendaji kwa mwaka pamoja na kupanga mikakati ya Chama kwa Mwaka unaofuata ikiwamo kubuni namna nzuri ya kuwahudumia wanachama wake.
Mkunda ameeleza kuwa kwa mwaka huu mambo mbalimbali yanayowahusu Wafanyakazi wanachana na wasio wanachama katika sekta ya afya na serikali kwa ujumla yameshugulikwa huku mengine Chama kikiendelea kuyawasilisha ili kupatikana muafaka. Mambo hayo ni kama vile Kushughulikia Malimbikizo ya Malipo ya nauli na uhamisho kwa Watumishi hasa wa sekta zilizo chini ya TUGHE kwenye Halmashauri.
Aidha. TUGHE wanaishauri Serikali kulipa posho hizo kutoka Hazina kama inavyofanya kwa waalimu badala ya utaratibu wa kutumia vyanzo vya ndani vya halmashauri kama ilivyo sasa.
TUGHE imeshauri pia serikali kuwalipa posho ya madaraka wakuu wa vituo vya afya kama inavyowalipa walimu wakuu.
Katika kuboresha maslahi ya watumishi wa Afya, TUGHE wameishauri serikali kufanya maboresho ya Posho ya kuitwa kazini (On call allowance) ambazo hazikufanyiwa maboresho wakati serikali inaboresha posho za kujikimu na posho za malipo ya masaa ya ziada.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu ameiomba Serikali kuendelea kufungua milango ya majadiliano na Vyama vya Wafanyakazi ikiwemo TUGHE kupitia mabaraza ya wafanyakazi ili kupata nafasi ya kuzungumza, kushauriana na kukubaliana kwa pamoja namna gani wanaweza kutatua changamoto zinazowakabili Wafanyakazi nchini na hatimaye waweze kupata haki zao wanazostahili.
Mkutano huo wa Baraza Kuu uliofunguliwa leo utafanyika kwa siku mbili ambapo umehudhuriwa pia na Makamu Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Cde. Jane Madete, Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake TUGHE Taifa, Cde. Catherine Katele, Katibu Kamati ya Wanawake TUGHE Taifa, Wajumbe wa Kamati ya Utendaji Baraza Kuu, Wajumbe kutoka katika mikoa yote ya Tanzania Bara pamoja na Watendaji wa TUGHE.