Marekani imetoa msaada wa dola 100,000 (Tsh. milioni 250.5) katika juhudi za kukabiliana na maafa yaliosababishwa na mafuriko pamoja na maporomoko ya ardhi yaliyotokea Wilayani Hanang Mkoa wa Manyara na kusababisha vifo vya zaidi ya Watanzania 70, kuharibu mashamba, na maelfu ya Watu kuyahama makazi yao.
Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umesema msaada huo unaotolewa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), kupitia Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, utasaidia Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na maafa yaliyotokea Manyara ambapo imesema USAID na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa nchini Marekani (CDC) vitaendelea kufuatilia hali hiyo na kutoa usaidizi wa ziada unapohitajika.
Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Michael Battle amesema “Tunaomboleza pamoja na Watanzania kote nchini kutokana na mafaa haya yaliyosababisha upotevu wa maisha pamoja na makazi, Wafanyakazi wote kutoka Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania tunawaombea wale wote walioathiriwa na mafaa haya”
“Marekani inasimama na Rafiki na Mshirika wetu Tanzania wakati huu, Serikali ya Marekani inaipongeza Serikali ya Tanzania kwa uongozi wao madhubuti na hatua za haraka za kupunguza athari za mafaa na kusaidia Wananchi katika Mkoa wa Manyara.