Rais wa zamani wa Sierra Leone ameitwa kuhojiwa na polisi kuhusu mashambulizi ya hivi majuzi ambayo maafisa wanasema yalikuwa mapinduzi yaliyoshindwa, afisa mmoja alisema Alhamisi.
Polisi walimwita rais wa zamani Ernest Bai Koroma hadi makao makuu yake “kuhojiwa juu ya jaribio lililoshindwa la mapinduzi” mnamo Novemba 26, waziri wa habari Cherno Bah alisema katika taarifa.
Koroma, ambaye aliongoza taifa hilo la Afrika Magharibi kwa miaka 11 hadi 2018, ametakiwa kufika katika idara ya uchunguzi wa uhalifu katika mji mkuu, Freetown, ndani ya saa 24, wizara ya habari ilisema.
Wito wake unafuatia kukamatwa kwa aliyekuwa msaidizi wake wa usalama.
Makumi ya watu waliojihami kwa bunduki walifanya shambulizi kali mwezi uliopita mjini Freetown ambapo walivunja ghala kuu la silaha la Sierra Leone na kuingia gerezani, na kuwaachia huru zaidi ya wafungwa 2,000.
Takriban wanachama 18 wa vikosi vya usalama waliuawa wakati wa mapigano hayo, huku zaidi ya washukiwa 50 – ikiwa ni pamoja na maafisa wa kijeshi – wamekamatwa hadi sasa.