Kipa wa Barcelona, Marc-Andre ter Stegen amefanyiwa upasuaji ambao klabu hiyo imeeleza kuwa “uliofanikiwa” kwenye jeraha la mgongo ambalo limemlazimu kukosa mechi za hivi majuzi.
Ter Stegen hajaichezea Barca tangu kabla ya mapumziko ya kimataifa ya Novemba na utimamu wake ulikuwa unatathminiwa mchezo hadi mchezo, ikitegemea maumivu na usumbufu wa mgongo wake.
Uamuzi wa upasuaji wa kutibu tatizo hilo awali ulichelewa lakini sasa umefanyika.
“Mchezaji wa kikosi cha kwanza Marc ter Stegen amefanikiwa kufanyiwa upasuaji kutokana na matatizo yake ya kiuno,” Barca walithibitisha Ijumaa asubuhi.
Operesheni hiyo ilifanywa na Dk. Amelie Leglise chini ya usimamizi wa wafanyakazi wa matibabu wa Barca katika kliniki karibu na Bordeaux nchini Ufaransa.
Klabu haijaweka hadharani muda wowote wa kutokuwepo kwa Ter Stegen, zaidi ya “kupona kwake kutaamua kupatikana kwake”.
Ripoti za awali wakati Barca walikuwa wanachelewesha uamuzi wa kuchagua kufanyiwa upasuaji au la, zilipendekeza kwenda chini ya kisu kutamaanisha kukaa nje kwa miezi miwili.