Mashindano ya robo mwaka mchezo wa Pool Table upande wa Black Ball yamekamilika jijini Dodoma na kuishuhudia klabu ya The Snipers ikiibuka na ushindi kwa kuifunga Moro Pool Club kwa fremu 13-10.
Mchezo huo wa fainali ulionekana kuwa wa kuvutia na wenye ushindani mkali kutokana na ubora wa timu zote mbili.
Mara baada ya kutwaa ubingwa huo, The Snipers Pool Club, wamejinyakulia Kikombe, medali, pamoja na fedha taslimu shilingi milioni moja na laki tano, huku washindi wa pili Moro Combine wakijinyakulia medali, pamoja na fedha taslimu shilingi milioni moja.
Mlezi wa TAPA Mrisho Mpoto maarufu Mjomba ndie aliyefunga mashindano hayo na kwa kuwakabidhi washindi zawadi katika mashindano hayo yaliyofanyika kwa muda wa siku tatu.
“Nimefurahishwa na viwango vizuri vilivyooneshwa na wachezaji zaidi ya mia moja na sitini walioshiriki katika wachezaji binafsi pamoja na timu kumi na sita kutoka mikoa sita ya Tanzania Bara pamoja na Visiwani Zanzibar, yamekuwa ni mashindano mazuri kwasababu wote mmekuja kushindana” alisema Mjomba.
Mashindano ya Robo mwaka yalizihusisha klabu mbalimbali za mchezo wa Pool zikiwemo Shooters Pool Club-Kinondoni, Kikuyu Kings Pool Club-Dodoma, The Warriors Pool Club-Dodoma, Skylight A Pool Club-Temeke, Skylight B Pool Club-Temeke, Vegas Pool Club-Kinondoni, na Moro Combine Pool Club-Morogoro.
Klabu nyingine ni Tip Top Pool Club-Kinondoni, TMK Waturuki Pool Club-Temeke, Mbeya Combine Pool Club-Mbeya, Zanzibar Combine Pool Club-Zanzibar, Iringa Combine Pool Club-Iringa, No Pot Pool Club-Arusha, Masti Pool Club – Ilala, na Legends Pool Club-Dodoma.
Kwa upande wa Wachezaji binafsi Wanaume Melickzedeck Amadeus amefanikiwa kutwaa ubingwa huo na kujinyakulia Kombe, Medali, pamoja na fedha taslimu shilingi laki saba na nusu, mshindi wa pili kutoka klabu ya TIP TOP Godfrey Mhando aliepoteza kwa fremu 9-2 katika fainali akajinyakulia fedha taslimu laki tatu na nusu.
Mashindano ya Swachezaji binafsi yalihusisha pia Wanawake waliocheza kwa mfumo wa ligi na kumshuhudia Grace Shindika akiibuka mshindi wa kwanza na kujinyakulia fedha taslimu laki mbili na nusu.
Nae Mwenyekiti wa Tanzania Pool Association TAPA Wilfred Makamba alisema kwamba lengo la Chama hicho ni kuuona mchezo wa Pool unastawi maeneo mbali mbali hapa nchini.